Add caption |
Loved One |
Watu wengi sana hawajui maana halisi ya upendo. Na tatizo linakuwa kubwa maana kuna aina nyingi za upendo ambazo si upendo halisi (Upendo wa kinafiki; mimi ninauita upendo feki) Kutokana na watu wengi kutojua maana halisi ya upendo, hivyo wengi wao huchanganya tamaa au mvuto wa mtu wakidhani ndio upendo. |
Hebu nikupe mfano
kidogo;
Unaweza ukamsikia
kijana anasema “Nilipomuona tu kwa mara
ya kwanza yule binti au mvulana, siku ile ile nilimpenda sana” Wenzetu
wameita “Love at First Sight”. Huu ni
upendo feki. Na vijana wengi sana huchanganya upendo na mvuto. Ukweli ni kwamba
wewe umevutiwa na huyo binti au huyo kaka, lakini si kwamba umempenda. Kwa
sababu kwanza humfahamu vizuri, hufahamu tabia yake, hufahamu anapendelea nini
au hupenda kufanya nini na vilevile bado hufahamu udhaifu alionao katika maisha
yake ya kila siku, lakini pia hufahamu hata afya yake kwa undani.
Upendo si hali ya
kuridhika tu moyoni umwonapo mtu, si kuvutiwa na umbo, mwendo au macho ya mtu.
Kupenda ni zaidi ya hapo. Upendo ni kuwa tayari kwa lolote na ili kuutunza
upendo, ni lazima ujue gharama zake na uwe tayari kuingia gharama hizo.
Kama hujui gharama za
upendo, huwezi kupenda. Ukijidai unapenda, ukikutana na gharama unazotakiwa
kulipa, inawezekana usiwe tayari kugharimika. Na usipokuwa tayari kuingia
gharama, hakuna upendo hapo, ni ubabaishaji tu. Japo wakati mwingine unaweza
ukawa na hisia kali za kutamani uwe naye. Upendo umebeba maana nzito, kubwa na
yenye thamani kubwa mno. Hivyo upendo hauanzi kwa kukurupuka tu, umemwona mtu
siku moja, mbili au tatu eti unasema unampenda. Nijuavyo mimi upendo huhitaji
muda na mara nyingi huhitaji majadiliano ndani ya nafsi ya mtu na pia upendo
hukua. Ninaposema upendo hukua maana yake ni kwamba, upendo huongezeka kadiri
unavyotambua thamani na ubora wa huyo umpendaye.
Kutambua thamani ya
umpendaye husababisha majadiliano ndani ya nafsi yako. Maana unapiga mahesabu
na kulinganisha kati ya faida na hasara za kuwa naye au kutokuwa naye. Hii
inakwenda sambamba na utayari wa ndani ya moyo; wa kukubaliana na udhaifu wake,
ili kufurahia mazuri aliyo nayo. Lakini si hivyo tu bali pia ni lazima umkubali
hata kama atabadilika hapo baadaye. Pia
unakuwa tayari kumsaidia katika udhaifu wake. Kwa kuzingatia hayo unaweza
angalau kupata picha ya upendo ni nini hasa.
Ngoja nikueleze kwa
namna nyingine ili uelewe vizuri tofauti kati ya upendo na mvuto. Ukiwa na
rafiki ambaye wewe unaona kuwa unampenda, na katika kuishi naye ukagundua kuwa
ni mvutaji wa sigara au mlevi sana, halafu huo upendo wako kwake ukafa, uwe na
uhakika hukumpenda ila ulivutiwa naye. Na pengine ulivutiwa na tabia ya
kutolewa au ya kutovuta sigara. Na ikiwa ulimpenda mwenzako alipokuwa na pesa
zilipoisha na upendo ukaisha uwe na uhakika hukumpenda ila ulivutiwa na aina ya
maisha yake au ulivutiwa na pesa zake. Inawezekana umekwishasikia kijana
akisema ‘yule binti katulia, mpole kwa kweli mimi nilipomwona tu
nilimpenda sana’ Ukweli ni kwamba huyo asemaye hivyo, hajampenda ila
amevutiwa na tabia ya utulivu na upole wa huyo binti. Ikiwa huyo binti
atabadilika na kuwa mkali au jeuri ni rahisi sana kumchukia kwa sababu kile
alichovutiwa nacho hakipo, yaani ule upole na
utulivu.
Na ndiyo maana mara
nyingi mahusiano mengi huvunjika baada ya muda fulani wa mahusiano. Hii ni
baada ya ama wote wawili au mmojawapo kugundua kuwa mwenzake ana tabia ambayo
yeye hawezi kuivumilia na hivyo ni vema kuachana na huyo mpenzi wake. Kumbuka
Biblia inasema upendo huvumilia. Sasa kama umeshindwa kuvumilia maana yake huo
haukuwa upendo, ila inawezekana ulikuwa mvuto tu. Sisemi kuwa uvumilie tu na
kuolewa au kumuoa mtu, hata kama hujaridhishwa na tabia yake, ila nazungumzia
kumpenda.
Kumpenda mtu si lazima
umuoe au uolewe naye. Ila kwa waliokwishaoana, hakuna sababu ya kuwatenganisha
isipokuwa kifo. Kwa hiyo unaweza ukaona umuhimu wa kujua nini maana ya upendo
na undani wa mahusiano kabla ya kuingia katika ndoa.
Ni vema nikueleze hili
kwa undani kidogo. Maana linaweza likawa gumu kwako au inawezekana likakuumiza
na hata kupelekea kumchukia rafiki yako aliyekuacha, hasa unaposoma kitabu hiki
na kuona kumbe alikuwa hakupendi ila kavutiwa tu na wewe. Na pengine
amekupotezea muda wako au amekuharibia maisha yako n.k. Ni hivi; Si wote wanaovutiwa na mtu fulani
wanakuwa wanajua kuwa wanavutiwa, wengine huwa hawajui, wao hudhani ni upendo,
na huwa na mtazamo wa kuwa marafiki wa kweli na hata kufikiri juu ya ndoa. Huwa
na hisia na msisimko nafsini mwao wakiwa katika urafiki huo. Lakini ghafla wanapogundua
tabia fulani kwa marafiki zao, ambayo haimpendezi, basi ile hali ya kutamani
kuendelea na huo urafiki inakufa. Tamaa au hawaa isipopata kile inachohitaji,
hufa mapema.
Hisia husababishwa na tafsiri
yako juu ya vitu. Hisia nzuri husababishwa na vitu unavyopenda, na hali
kadhalika hisia mbaya husababishwa na vile unavyovichukia. Kupenda kitu (yaani ‘like’)
na kuchukia kitu (yaani ‘dislike’) ni matokeo ya tafsiri uliyonayo juu ya vitu
hivyo ambay hutokana na kiwango chako cha uelewa au ufahamu wa mambo. Ndiyo
maana nikakwambia kupenda si hisia ni zaidi ya hisia. Maana inawezekana ukawa
unapendezwa na tabia, macho ya mtu, miguu, umbile lake au kazi yake au namna
anavyovaa. Vikikosekana hivyo vitu kwa huyo mtu uwe na uhakika na hiyo hisia
yako nzuri inatoweka, japo mtu ni yuleyule; hajabadilika. Upendo haungalii
hivyo tu, ila ni zaidi ya hapo, unampenda mtu na si mwili wake au mavazi au
mali zake, japo ni vizuri vikikuridhisha pia.
Marafiki ambao
huongozwa na hisia, wakiona vile vinavyowachukiza, wanakuwa hawajisikii tena
kuendelea na uhusiano. Na wengine wao huwa na hasira sana. Hii ni kutokana na
yeye kuona ule mtazamo aliokuwa nao na ile ndoto haitimii kama alivyopanga
akilini mwake au kama hisia zake zinavyotaka. Maana yake ni kwamba alifanya
uamuzi wa kuwa na uhusiano huo kwa kuongozwa na hisia zake pamoja na mvuto
alionao huyo rafiki yake. Sasa kama nilivyokueleza hapo mwanzo kuwa, ule mvuto
ukitoweka au ukichanganyika na kitu ambacho hakikuvutii ile hisia na hamu ya
kuendelea na uhusiano inapungua au inaweza kutoweka kabisa.
Mara nyingi vijana
hudanganyana kwa kuambiana nakupenda lakini hawajui nini maana halisi ya
upendo. Wakati mwingine wanakuwa na upendo wa kinafiki. Si kwa sababu upendo ni
kitu kigumu, ila ni kwa sababu ya kukosa maarifa na uelewa wa kutosha juu ya
maana halisi ya upendo na chanzo cha upendo “Watoto wadogo, tusipende kwa neno wala kwa ulimi, bali kwa tendo na
kweli” 1 Yoh 3:18
Kutoka kitabu hiki cha 1 Yoh 3:18 Yohana anaonya na
anatuonyesha aina feki ya upendo ambayo vijana wengi hawatambui. Yohana pia
anajaribu kutuonesha namna au jinsi ya kupenda. Kuna kupenda kwa “neno” au
kupenda kwa “ulimi”. Ni vigumu kutambua ukweli wa maneno unayoambiwa na mtu au
rafiki yako kwamba yanatoka ndani ya moyo wake yaani anamaanisha au ana ajenda
nyingine ya siri. Pamoja na ugumu huo uliopo katika kutambua ukweli wa maneno,
vijana wengi huamini au hushawishika kwa maneno tu hata kama hawajaona matendo.
Ila ni vema ufahamu kuwa yatupasa kupenda kwa “tendo” na “kweli”.
Upendo unapaswa uwe wa
matendo mema na kweli. Kufanyiwa matendo mengi hata kama ni mazuri kiasi gani,
kama hakuna ukweli ndani yake basi na upendo haupo. Maana ni rahisi sana
kuingia katika upendo feki kama hujui kuwa katika matendo lazima kuwepo na KWELI. Wengi wamekuwa wakitamka maneno
mazuri na wakiwafanyia wenzao matendo mazuri ili ionekane kuwa wanawapenda, na
kumbe kweli haimo ndani yao, ni unafiki mtupu. Kufanyiwa matendo mazuri au
kumfanyia mwenzako matendo mazuri pasipokuwa na kweli ndani ya moyo wako,
haitoshi kukamilisha upendo. Inawezekana
unafanyiwa mambo mengi mazuri, ila omba kusudi la Mungu lisimame. Sisemi uache
kumwamini rafiki yako, ila nataka ufanye maamuzi ukiwa makini na ukijua siri
hii ya upendo na si kupumbazwa na mambo mazuri unayofanyiwa. Bali kweli ya
Kristo iwepo katika uhusiano wenu.
Ili kijana uwe na uwezo
wa kufanya maamuzi sahihi na kuwa na ufahamu juu ya mahusiano yako na watu
wengine hasa wa jinsia tofauti na wewe ni lazima uwe na Roho Mtakatifu. Pasipo
Roho Mtakatifu, hakuna kitakachoonekana rahisi. Na mara nyingi utafanya maamuzi
ambayo si sahihi, utajeruhiwa na inawezekana ukakata tamaa kabisa, na mfumo
mzima wa maisha yako ukaharibika. Wengi hujuta na kuishia kulaumu maamuzi yao
au kulaumu marafiki zao. Roho Mtakatifu
hutufundisha hivyo tunapata maarifa, ufahamu na hekima ya kufanya mambo yetukatika maisha yetu.
Hii ni sehemu tu yakitabu changu kiitwacho "UPENDO UPITAO UFAHAMU" ambacho kipo mbioni kuchapwa kinasubiri fedha tu. Naomba maoni yako. Asante
Dk. George Adriano
Simu: 0715 182 106
Tanzania
Nice article! Be blessed daktari
ReplyDelete