Hili ni Jina tarajiwa la Kitabu Kitarajiwa |
..........Kiongozi anayeona mbele
na asiamini anachokiona na asipokuwa na nia ya kutaka kufikia yale mazuri
ayaonayo mbele yake, hafai kuwa kiongozi. Haina maana kuwa na maono pasipo
msukumo wa kuyafikia maono hayo. Wapo viongozi wa aina mbalimbali kwa namna
walivyo.
1. Viongozi Wanaotumia Madaraka
Kufanikisha Mambo Yao
Wapo viongozi wenye
ushawishi mkubwa hasa wa kisiasa na wanaonekana kuwa na maono. Wapo viongozi si
tu wanaonekana kuwa na maono lakini pia wanaonekana kuwa na uwezo wa
kuwafikisha wenzake kule anapopaona. Mara nyingi hufanya mambo makubwa na
wakati mwingine kwa ujasiri sana lakini ndani yao hawaoni maisha ya wengine
bali maisha yao pekee. Viongozi wa aina hii hawatambuliki mwanzoni ila baada ya
muda hutambulika tu kuwa msukumo ulio ndani yao si kutetea wanyonge ila ni kwa
ajili ya matumbo yao.
Hupenda sifa na
kuonekana na watu. Mara nyingi hawapotezi nafasi ya kujionesha kwa wananchi au
jamii yake hata kwa mambo madogo. Hupenda kuonekana kuwa wanapenda watu na
hujichanganya na watu ili waonekane wazuri sana.
Si ajabu ukimkuta
akimpa fedha ombaomba barabarani au akimpa fedha mtoto wa mtaani anayeombaomba
barabarani pasipo hata kujua kama kweli ni yatima au la! Kwa watu makini
wanaoelewa nini maana ya uongozi, kwamba ni kuwa na uwezo wa kuona mbele zaidi
ya wengine na kuwa na uwezo wa kuwashawishi kufikia huko mbele, watakubaliana
na mimi kuwa kiongozi yeyote anayefanya hayo hana tofauti na raia wake. Maana
raia wa kawaida vilevile huwapa fedha ombaomba hao wanaoketi kandokando mwa
barabara. Sasa tofauti yake na wananchi wake ni ipi? Tofauti inawezakuwa ni
lengo la kufanya hivyo. Wakati kwa kaisi kikubwa mwananchi anaweza kumpa fedha
kidogo ombaomba kwa lengo la kumsaidia lakini kwa kiongozi huyu yeye atataka
pia aonekane mwema, ndiyo maana hutaka kupigwa picha na kutangazwa. Kwa maneno
mengine anasisitiza watu waendelee kuombaomba au anakubaliana na watoto
wanaozurura mitaani kuendelea kuombomba pasipo kutafuta suluhu ya kudumu.
Na mara nyingi anapotoa
fedha, lengo lake si kutatua tatizo au kumsaidia yule anayeomba ila lengo lake
ni kujionesha kuwa mwema. Kujionesha kuwa yeye ni mtu wa watu ili aendelee
kujinufaisha yeye na familia yake. Kuwa mtu wa watu katika kuwasaidia kwa dhati
katika njia stahili ukiongozwa na dhamira ya kweli na iliyo thabiti ni sawa
lakini si katika unafiki ili utimize tamaa yako binafsi. Nikuhakikishie hivi,
kiongozi yeyote au mtu yeyote anayependa kuonekana mwema machoni pa watu hafai
kuwa kiongozi hata kwa kikundi kidogo cha watu wachache. Hutafuta kuonekana wazuri ili wapate sifa na
nafasi ya kunyonya wengine.
Ninazungumza
niliyoyaona mwenyewe, si ya kuambiwa wala kuhadithiwa. Nimekuwa nikifuatilia
hili kwa miaka nane sasa. Mtu yeyote anayefanya mambo mazuri kwa lengo la
kujionesha kwa watu kuwa mwema mara nyingi huwa si wema. Mara nyingi huwa na
ajenda yao wanayoijua wao. Na hata kama hawana ajenda yoyote nyuma ya hayo
wanayoyafanya lakini matokeo ya nilivyofuatilia yanaonesha kuwa bado huwa si
watu imara, si watu thabiti na makini kuwa viongozi.
Viongozi katika kundi
hili mara nyingi huwa ni wezi. Mara nyingi utasikia wameficha fedha nje ya nchi
au wameweka fedha nyingi katika mabenki ya nje ya nchi zao. Nikuhakikishie pasi
na shaka kuwa kiongozi yeyote mahala popote duniani anayeweka fedha nje ya nchi
yake hata kama ni fedha zake halali kabisa, bado hafai kuwa kiongozi. Huyo hana
uchungu na Taifa lake, hana uchungu na watu wake, hana uchungu na watu wa nchi
yake na kwa hakika si mzalendo hata kidogo. Baba anayejali familia yake hawezi
kufanya mambo yanayonufaisha jirani huku wanawe wakihangaika kwa njaa. Kiongozi
mwenye uzalendo na nchi yake hawezi kujenga hoteli za kifahari nje ya nchi na
asijenge katika nchi yake mwenyewe.
Viongozi au watawala wa
aina hii, huwa na maisha ya kifahari wao na ndugu zao. Ama mkewe, au wanawe na
hata mashemeji wanaweza kuwa matajiri wa kupingukia na mara nyingi hupata fedha
zao kiujanjaujanja tu; huwezi kueleza au kuonesha wazi miradi au biashara
wanazofanya. Na kama wanafanya biashara, basi utashangaa maana biashara zao
mara nyingi huwa haziendani na utajiri walio nao. Na hata katika biashara
hufanya kwa mbinu mbalimbali wakikiuka taratibu au sheria za nchi kwa mufaa
yao. Unakuta mtoto wa rais mathalani, ana biashara za kawaida tu ambazo hata
watu wengine wanazo lakini yeye ni milionea.
Na kama utaweza
kuchunguza walivyopata madaraka ni mara chache utakuta wamechaguliwa kihalali.
Mara nyingi hutumia mbinu mbalimbali wanazozijua wao ili kupata madaraka. Si
vibaya nikizungumzia mbinu chache ambazo zinaweza kutumika kupata madaraka ili
watekeleze ajenda zao. Sasa si lazima mbinu au njia zote nitakazoeleza hapa
zitumike lakini nataka ujue na uwe makini na mambo yanaweza kuangamiza Taifa
lolote lile duniani, lakini hasa katika nchi za Afrika.
Hutumia
Propaganda
Propaganda hutumiwa
sana hata katika mataifa makubwa duniani. Propaganda za kitoto na hata za
kijinga hutumika sana katika nchi zinazoendelea kama Tanzania. Propaganda hizi
huwa haziwezi kufanya kazi katika mataifa yaliyoendelea. Hizi hufaa kwa
wananchi wajinga. Nchi zinazoendelea na zenye watu werevu wa kutosha huhitaji
utaalamu na umakini mkubwa katika kuhakikisha propaganda inafanya kazi
iliyokusudiwa.
Viongozi wa aina hii hupenda
kuonekana wazuri kwa kutumia gharama za wengine. Hutumia gharama za wengine kwa
maana ya kuwafanya wengine waonekane wabaya ila yeye aonekane mzuri na anafaa. Na
mara nyingi hiyo huwa propaganda tu.
Hutumia njia mbalimbali
kufikia katika adhma yake ya kutukuzwa. Pamoja na njia nyingine lakini hutumia
propaganda kuwachafua wengine au kuwasema kuwa ni dhaifu. Kiongozi wa aina hii
huwa....
Nitaendelea nikipata maoni ya waasomaji.... maana kuna vitu sensitive ....
Dk. George
0 comments:
Post a Comment