Kuwa na uhusiano ni
mwanzo wa kuwajibika zaidi. Maana uhusiano unahitaji kujengwa na kutunzwa ili
uwe imara zaidi. Mahusiano mengi huvunjika au huwa si mazuri, kwa sababu wengi
hudhani kuwa ukimpata rafiki kinachofuata ni kufurahia uhusiano. Sawa! Lakini ni
lazima ujue kuwa ni lazima kuwajibika zaidi ili thamani na ubora wa uhusiano
wako udumu na uzidi kukua. Yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia
katika kujenga na kuuimarisha uhusiano mzuri.
i.
Upendo
Upendo ni kitu muhimu
na cha thamani sana katika uhusiano wowote duniani. Maana hata uhusuiano wetu
na Mungu umejengwa katika upendo. Upendo ni kifungo cha ukamilifu. “Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio
kifungo cha ukamilifu” Wakolosai 3:14
Pasipo upendo hakuna uhai wala maisha. Maana Mungu ni Pendo. Upendo uliokamili
tumepewa na Mungu mwenyewe. “…na tumaini
halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo
yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa” Rumi
5:5 Kwa maneno mengine tunapokuwa na Roho Mtakatifu, upendo wa Mungu
huwa katika mioyo yetu. Wapo watu ambao hujionesha kuwa wamejazwa Roho
Mtakatifu, ila upendo hawana. Kumbuka suala si kuwa na roho ila ni roho ya
namna gani uliyonayo.
Ni vema kuwa muwazi kwa
mwenzako, shirikishaneni mambo yenu katika maisha yenu. Inawezekana ni mambo
yaliyopita au yaliyopo au yajayo. Wengine huficha na hata kusema uongo juu ya
maisha yao ya nyuma kabla ya uhusiano huo, wakidhani ni kujenga uhusiano. Sivyo
hata kidogo, kufanya hivyo ni kuubomoa uhusiano wako. Ukifanya hivyo, maana
yake ni kwamba humuamini mpenzi wako au hujui maana ya upendo (humpendi). Ni
vema kuwa makini hapa, maana ni lazima uwe na ufahamu wa ki-Mungu na ujue ni
lipi la kusema kwa kiwango gani na wakati gani, na kwa nani. Uwe na ufahamu wa
kuwatambua marafiki kwa aina zao. Maana unaweza kujikuta unaeleza mambo yako
muhimu kwa mtu ambaye hana mpango wowote na wewe, na pengine anaweza akakuumiza
sana.
Kumbuka upendo
haubadilishwi na kitu chochote. Kwa hiyo kama mtu anadai kuwa anakupenda lakini
ukimwambia mambo yako yaliyokutokea hapo nyuma naye akaona kuwa ni mabaya na
hawezi kuwa na wewe tena, uwe na uhakika alikuwa hakupendi, ila anayapenda
mambo yako ya sasa. Na pengine tafsiri yake au uelewa wake juu ya upendo ni
finyu. Wahenga walisema, usione vyaelea vimeundwa. Maana yake, kila kitu kina
gharama yake, na ukiona kitu kizuri jua ipo gharama iliyosababisha uzuri huo.
Hapa sina maana uropoke kila kitu kilichokwishapita, ila ikiwa rafiki yako
atakuuliza kitu, sema kweli maana uongo si tu unaharibu uhusiano wenu ila pia
ni dhambi, na hii humpa Ibilisi nafasi ya kuwashambulia. Kila neno lina muda
wake unaofaa kunenwa. “…neno linenwalo
wakati wa kufaa ni jema kama nini!” Mithali
15:23
Wengi hudhani ikiwa
uongo waliosema hautajulikana, basi watakuwa salama. Si hivyo hata kidogo. Ubaya
wa uongo na athari zake zipo pale pale, haijalishi uongo huo umejulikana au la.
Hebu tusome vizuri maandiko; “Shahidi wa
uongo hakosi ataadhibiwa; naye asemaye uongo ataangamia” Mithali 19:9 Shahidi wa uongo ataadhibiwa, kwa nini? Ni kwa
sababu ameonekana na uongo wake umejulikana, kwa hiyo anaweza kuadhibiwa.
Lakini asemaye uongo ataangamia, sio ataangamizwa na tena sio ataadhibiwa.
Inawezekana ikawa ngumu kumuadhibu, maana inawezekana uongo wake haukujulikana,
kwa hiyo hata kuangamizwa inaweza ikawa ngumu pia. Biblia inasema ataangamia;
nini kitamwangamiza? Bila shaka ni uongo aliousema.
Ibilisi ndiye baba wa
uongo. Ukisema uongo maana yake unajikabidhisha au unajihalalisha kuwa mtoto
wake. Wengi hawajui hili, wanajua tu kwamba uongo ni dhambi, basi. Sawa! Ila
tangu leo tambua siri hii itakusaidia sana. Unaposema uongo, hata kama
haitajulikana kwamba ulidanganya, utakuwa tayari wewe ni mtoto wa Ibilisi,
aliye baba wa uongo. Uongo kamwe hauokoi urafiki au uhusiano wako, bali uongo
unaangamiza kila kitu chema.
Masuala yanayohusu
mahusiano mliyokuwa nayo kabla ya ninyi kukutana si vema sana kuyazungumza.
Maana mara nyingi masuala hayo huendeshwa kwa hisia. Hata hivyo masuala
yanayohusu uhusiano uliokuwa nao au aliokuwa nao rafiki yako, huwa hayana
msaada sana. Hakuna haja ya kujiongezea taarifa za kuumiza, wakati hazina
msaada. Ila kama zinahitajika kwa ajili ya kujenga uhusiano wenu wa sasa
mnaweza kuzungumza. Mambo ya mahusiano yaliyopita au yaliyovunjika kabla ya
uhusiano wa sasa yatumike na mtu binafsi katika kulinda na kutunza uhusiano
alionao sasa, lakini ni vema kuepuka kuyajadili. Jifunze kutokana na makosa
yaliyotokea katika urafiki uliopita.
Matatizo au kasoro zenu
katika uhusiano wenu wa sasa, msiziache pasipo kuzitatua. Zitatueni haraka na
mapema iwezekanavyo, ili kasoro hizo zipone. Na kama zitabaki basi labda yawe
makovu, lakini si vidonda. Maana kidonda huuma lakini kovu haliumi. Haijalishi
ni muda gani umepita kama kidonda hakijatibiwa na kupona, maumivu yataendelea
kuwapo. Na kidonda chaweza kuongezeka, maumivu yakawa makali zaidi, ikawa ngumu
hata kutibika. Ni vema ujue kuwa ikiwa kuna mambo hamtayatatua katika uhusiano
wenu au ndoa yenu, yanaweza kuwasumbua hapo baadaye hata miaka kumi na mitano
(15) ijayo. Uwe makini sana katika kutunza uhusiano au ndoa yako. Si jambo gumu
unahitaji ufahamu na uelewa tu. “Yesu
akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye” Marko 9:23
Katika upendo uwe tayari kuwa na rafiki yako
katika maisha yako yote. Upendo si hali ya kujisikia uchungu kwa namna ambayo
unaona kana kwamba umeonewa au kufanyiwa isivyostahili. Na kamwe, upendo si
kuwa na hasira. Upendo husababisha aina fulani ya furaha ndani ya mtu pale
unapomtendea mtu mambo au jambo jema, bila kujali yeye amekufanyia nini au
atakufanyia nini hapo baadaye. Ni kweli unaweza ukapata maumivu ya..... Itaendelea Na Dk George Adriano
Tanzania
Semina ya Mwl Christopher Mwakasege viwanja vya Jangwani, DSM tar 24 Feb-03 Machi
0 comments:
Post a Comment