Ikiwa hukusoma sehemu ya Kwanza ni vema ufanye hivyo, maana sitatoa muhtasari hapa ili na wewe uchukue wajibu wako wa kujifunza...!
Upendo si hali ya
kujisikia uchungu kwa namna ambayo unaona kana kwamba umeonewa au kufanyiwa
isivyostahili. Na kamwe, upendo si kuwa na hasira. Upendo husababisha aina
fulani ya furaha ndani ya mtu pale unapomtendea mtu mambo au jambo jema, bila
kujali yeye amekufanyia nini au atakufanyia nini hapo baadaye. Ni kweli unaweza
ukapata maumivu ya mwili pale unapokuwa ukitenda mema hayo, lakini maumivu hayo
hayasababishi ujisikie uchungu wa hasira wala kufadhaika bali furaha ya ndani.
Hata unapotunza nafsi yako huwa unaingia gharama na wakati mwingine huwa
unaumia mwili wako.
“Lakini
kama mnavyoshiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu
wake mfurahi kwa shangwe. Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu;
kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia” 1 Petro 4:13-14 Mtume Paulo, anazungumza habari ya sisi
kushiriki mateso ya Kristo na kufurahi kwa wakati uo huo. Si jambo rahisi kuwa na furaha wakati wa
mateso, ni mpaka uwe na uelewa wa rohoni utokao kwa Mungu, yaani ufahamu wa ki-Mungu. Ndiyo maana Mtume Paulo anasema, kwa kuwa
Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia. Maana yake ni kwamba linafanyika jambo,
linakuumiza mwili au nafsi yako, lakini kwa wakati uo huo unakuwa na furaha
ndani yako. Furaha haisababishwi na maumivu unayoyapata bali inatokana na
ufahamu au uelewa utokao kwa Mungu, ulio nao ndani yako. Hauangalii mates ohayo
bali unaangalia kile chema ulichofanya. Kumbuka upendo haushindwi
na kitu chochote.
i.
Mawasiliano
·
Sikiliza
Mara nyingi urafiki na
wakati mwingine hata ndoa huvunjika au kukosa amani na furaha kwa sababu ya
mawasiliano mabaya. Wanapendana kabisa tena kwa dhati na kwa moyo wote, lakini
mawasiliano, hovyo. Msikilize mwenzako kwa umakini mkubwa, huku ukimtazama. Si
unatazama televisheni au unasikiza redio au unasoma kitabu au gazeti halafu
unamwambia ‘nakusikiliza endelea’. Ni vema kusikiliza kwa makini huku ukimtazama
mwenzako machoni ikibidi. Hii humpa hamasa anayezungumza, kuendelea kuzungumza,
hujisikia kusikilizwa na kuthaminiwa, hasa unapoacha kufanya ulichokuwa
ukifanya; ukiacha kusikiliza redio au kutazama luninga, kusoma kitabu au gazeti
halafu ukamsikiliza mwenzako ni vema sana, inabariki. Na wakati mwingine kama
mpo pamoja epuka kuchezea simu, kuandika ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu
yako au kupiga na kupokea simu mara kwa mara. Kama umeamua kutoka na rafiki
yako basi ikiwezekana zimeni simu zenu. Haileti picha nzuri wakati unaongea na
mpenzi wako yeye anapokea simu au anasoma ujumbe wa simu n.k.
Katika kusikiliza kuna
namna nyingi za kusikiliza. Kuna mtu anasikiliza ili tu aonekane anasikiliza.
Mwingine anasikiliza kwa lengo la kusubiri nafasi yake kujibu au aongee. Wapo
wanaosikiliza ili tu umalize kuongea, na pia wengine husikiliza kwa sababu ni
wajibu kusikiliza. Lakini unapaswa kusikiliza kwa lengo la kuelewa uhalisi wa
unachoelezwa kama vile yule anayekueleza anavyoelewa. Yaani unajitahidi uelewe
kama yeye. Maana ukielewa tofauti na anachomaanisha inakuwa haina maana sana.
Kuelezwa na kusikiliza kwako vyote ni kazi bure. Maana hata utakavyojibu
haitakuwa sawa sana maana hukuelwa kama alivyokusudia, rafiki yako.
·
Subiri
Vilevile ni vema
usubiri mwenzako amalize kuzungumza. Si unamkatisha kuzungumza ukidhani kuwa
umekwishamuelewa, si tabia njema. Kutomkatisha mtu anapozungumza, si tu
humfanya mwenzako kujisikia kuthaminiwa, lakini pia kuna faida kubwa
kumsikiliza mtu mpaka anapomaliza kuzungumza. Hii hukusaidia wewe kutambua kwa
usahihi fikira, mawazo au mtazamo wa mwenzako juu ya jambo analozungumzia.
Hivyo kukupa wewe nafasi nzuri ya kuzungumza au kujibu kwa usahihi zaidi. Maana
kuna watu wengine hupenda kudakia wakati mwenzake akizungumza. Huko ni kukosa
utashi wa mawasiliano, lakini pia ni dalili ya ubinafsi na dharau japo si
lazima iwe hivyo. Maana yake ni kwamba unadhani wewe ndiyo upo sahihi kuliko
mwenzako, au huthamini anachokisema, unakidharau au unamdharau yeye mwenyewe.
Tabia hiyo inaweza kabisa kuharibu urafiki wako. Kumkatisha mwenzako kuzungumza
kufanyike pale tu inapodi, na hasa ikilenga ama kuepusha au kutatua tatizo
fulani.
·
Elewa
Pamoja na kusikiliza
hakikisha umeelewa. Unapomsikiliza mwenzako, jaribu kuomba ufafanuzi pale
ambapo hujaelewa ukionesha hisia za kuguswa, au msisimko wa kile
anachokieleza. Usisikilize tu ili
kutimiza wajibu. Ili kuonesha kuwa upo makini ukimsikiliza. Jaribu kutumia
maneno yanayoonesha kuwa upo makini; maneno kama vile, ‘unamaanisha nini hasa unaposema….’ au ‘ehe halafu ikawaje…?’ au ‘kwa hiyo na yeye aka…’ au ‘mmh, jamani, sasa ulifanyaje?’ au ‘hebu nieleweshe, kwa nini umeamua hivyo?’ n.k Hii inategemea
na aina ya mazungumzo na kinachozungumzwa. Wakati mwingine si vema sana kujibu
swali kwa kutumia swali. Swali lijibu swali inapobidi tu hasa katika kufafanua
au kufanya kitu au jambo lieleweke zaidi.
·
Eleweka
Unapoeleza kitu au
jambo jaribu, kufupisha lakini pasipo kupoteza maana ya ulichotaka kusema au
kueleza. Usizungumze hadithi ndefu kupita kiasi, hasa kama wewe si mtaalamu
mzuri wa kuhadithia katika mtiririko unaoeleweka. Hii inategemea na namna
rafiki yako alivyo au anavyopendelea. Maana unaweza kudhani kuwa unahadithia
vizuri, kumbe kila unavyozidi kuongea ndivyo unavyozidi kumchanganya mwenzako
na wakati mwingine kujichanganya hata wewe mwenyewe. Hii inaweza kuleta hisia
kuwa unachosema ni uongo au kuna jambo unaficha, ndiyo maana unazunguka zunguka
badala ya kueleza moja kwa moja. Eleza kwa ufupi, tena vitu muhimu vyenye
kujenga au vyenye mafunzo au changamoto ndani yake. Ili pamoja na kufurahi na
rafiki yako, lakini pia mjifunze mambo ya msingi ya kuboresha uhusiano wenu.
Ni vema utambue kuwa katika uhusiano hasa kwa
kipindi cha mwanzo hata jambo dogo lina maana kubwa katika uhusiano. Kusita
kueleza kitu, labda kwa sababu...... Itaendelea sehemu ya 3Nitafurahi kupata maoni, ushuhuda, maswali au ukinishirikisha jambo lolote. Hakuna gharama yoyote.
Na Dk George Adriano
Simu Na. +255 715 182 106
Nipo Dodoma kwa sasa.
NAKUTAKIA KAZI NJEMA HII AMBAYO MUNGU AMEKUITIA ,NIMATUMAINI YANGU WAPENDWA WENGI TUTAELEWA NAKUBADIRIKA
ReplyDeleteAmen, asante tuombeane ili Mungu aonekane na si mtu. Stay blessed
Delete