Friday, February 15, 2013

Spika Kulindwa Dhidi Ya Wananchi Tafsiri Yake Nini?

Ndugu zangu watanzania wapendwa, ni nani kati yetu asiyejua uzuri na utajiri wa nchi yetu? Tunaweza kujipongeza kwa nchi yetu kuweza kuwa na maajabu matatu ya asili yanayoingia katika maajabu saba ya Afrika. Kweli ni jambo jema ila moyoni mwangu ni kama ninanyogonyea na kujisikia vibaya. Wewe unajisikiaje?

Spika wa Bunge Anne Makinda Akila kiapo. Unadhani anaapa kutoka moyoni?
 
Mchangiaji mmoja katika gazeti la The Guardian la Uingereza siku za nyumba kidogo alisema “Tanzania ni nchi tajiri kuliko zote duniani kwa maliasili” Kumbe hili inafahamika sit u hapa Tanzania ila hata nje ya mipaka ya Tanzania. Tanzania ina eneo kubwa lenye rutuba kwa ajili ya kilimo. Tanzania ina mabonde na milima mizuri inayovutia na hata mlima mrefu kuliko yote Afrika yaani mlima Kilimanjaro upo hapa kwetu Tanzania.
Tanzania ina maziwa na mito ya kutosha ambayo  inaweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji. Hii siyo tu kwamba itatufanya kusahau njaa lakini itatuweka katika nafasi nzuri kiuchumi na hata kwasaidia majirani zetu kwa chakula.

Eneo kubwa la mashariki mwa nchi yetu limepakana na bahari ya Hindi. Bahari na maziwa haya yana utajiri mkubwa wa samaki, mafuta, gesi na viumbe wengine wa majini. Katika pwani ya Bahari ya Hindi tunazo bandari tatu ambazo bado zipo katika hali ya udhaifu na aibu kubwa. Bandari ya Mtwara, mathalani ni bandari yenye kina kirefu kuliko zote katika pwani hiyo. Lakini bado Afrika ya Kusini, Msumbiji na jirani zetu Kenya bandari zao ni bora mara dufu na zina ufanisi wa hali ya juu ukilinganishana zetu. Bandari zetu zimegubikwa na taarifa za ufisadi na ufisadi wa kutisha.
Tanzania ina mbuga za wanyama na hifadhi za Taifa lukuki. Watalii wa kutosha tu hufurahia mbuga na hifandhi hizi na wengine huja kwa ajili ya uwindaji. Hili ni eneo jingine tunaloweza kupata faida kubwa na kukuza uchumi wetu. Tanzania ni kisiwa cha mambo mengi ambayo hayapatikani popote duniani. Vyura wa Kihansi ni vyura pekee wanaopatikana Tanzania peke yake.

Madini tuliyonayo ni kama kufuru hivi. Achilia mbali dhahabu, almasi, chuma, makaa ya mawe, na urani lakini pia tuna Tanzanite. Madini ya Tanzanite hayapatikani au niseme hayachimbwi popote duniani  isipokuwa Tanzania. Makaa ya mawe yanayopatikana hapa kwetu ni bora zaidi ya makaa yanayopatikana Afrika ya Kusini kwa nishati.
Ziwa Victoria ni kubwa kuliko yote barani Afrika. Ziwa Tanganyika lina kina kirefu kuliko yote Afrika. Mbuga za Serengeti na Ngorongoro ni za kipekee kuliko zote barani Afrika, sasa zinaingia kwenye maajabu saba ya asili ya Afrika.
Bonde la mto Rufiji, Ruvu, Ihefu na mangine mengi ni mabonde yenye rutuba na mazuri ajabu kwa kilimo. Sasa tunayo gesi. Inaanza kuzua balaa badala ya baraka. Binafsi sidhani kama limetatuliwa ila limetulizwa tu. Korosho zinazozalishwa Tanzania ni korosho bora kuliko zote duniani. Tanzania tumekosa nini kwa Mungu?

Pamoja na kuwa na mali aslili zote hizi achilia mbali hizo ambazo bado hatujazigundua lakini kuna baadhi ya viongozi hata wa ngazi ya juu kabisa serikalini ambao huthubutu kutamka hadharani eti Tanzania ni masikini. Hii ni aibu kubwa. Ila dawa yake ni ndogo na kila mtanzania anafahamu.
Miaka 51 tangu tupate uhuru Tanzania imekuwa na uongozi, imekuwa na serikali na mali asili hizi pia zimekuwepo kwa muda mrefu. Unapoona kiongozi mkubwa wa nchi anatamka kuwa Tanzania ni masikini, maana yake ni rahisi tu. Maana yake ni kwamba upeo wa kuona mbele na kufikiri mbele umefika kikomo. Kwa namna yoyote ile hamtaweza kupiga hatua hata kidogo.

Ninaposema kukosa au kushindwa kuona mbele zaidi simaanishi kwamba kweli haelewi la hasha. Nina uhakika watawala wetu wote wanatambua, wanaelewa na wanaona utajiri wa nchi hii. Ila tatizo kubwa ni mfumo uliojengeka au uliojengwa na serikali hii iliyokaa madarakani kwa muda mrefu ikiongozwa na CCM. Mfumo umejengwa kwa namna ambayo huwezi kutumika kwa ajili ya jamii au kwa ajili ya maendeleo ya watanzania. Kufanya hivyo ni kosa kubwa katika mfumo wa chukua chako mapema.
Katika mfumo wa Chukua Chako Mapema, yeyote anayeingia katika mfumo huo, akiwa kiongozi ama mshirika ni lazime aukubali mfumo huo wa Chukua Chako Mapema. Kama hutaki kuchukua chako mapema basi huna budi kukaa kimya huku ukitumbua macho yako kutazama wenzako wakifanya hivyo.  Na siyo tu kukaa kimya na kuwaacha wenzako wachukue vyao (siyo vyao kweli ni vya wananchi) mapema ila ni lazima pia uwe angalau una uwezo mdogo wa kuwa mnafiki. Kuwa mnafiki kwa maana kwamba na wewe ufiche siri za wizi wa wenzako au usaidie wao kuiba. Maana utasikia “weee pitisha bwana dili ya mkubwa hiyo”

Lakini tabia nyingine ya mfumo mbovu katika nchi, haukuruhusu usimamie kweli, haukuruhusu ufanye kazi kwa bidiii na kwa maendeleo ya watanzania. Kufanya hivyo ni kuvunja kanuni na pia ni kujaribu kuweka hatarini siri wa wenzako na njia zao za kuchukua mapema. Kwa hiyo hata ukijaribu kukaa kimya, hata ukiamua kufanya kazi ya dhati kwa maendeleo ya Taifa, nina kuhakikishia vikwazo vyake ni vikubwa mno. Ni hatari sana kufanya kazi kwa uaminifu katika mfumo wa Chukua Chako Mapema.
Tunayo mifano hai, hakuna haja kuandikia mate. Nani haelewi anayokutana nayo Waziri Dk Harison Mwakembe? Nani hakumbuki au haelewi yaliyomkuta aliyekuwa Spika wa bunge lenye kasi na viwango, Mh. Samweli Sitta? Ili uweze kuonekana unafaa na upatiwe mapochopocho matamu kutoka katika mfumo wa Chukua Chako Mapema basi huna budi kuwatetea.

Na utapewa mapochopocho si utani. Mara ooh, spika wa bunge aongezewa ulinzi na kubadilishiwa magari. Hizi ni mabazo utazisikia kwenye vyombo vya habari ila si lazima usikie yote. Hii ni nchi pekee ambayo mtu anaweza kushindwa ubunge halafu akateuliwa kuwa balozi au mkuu wa mkoa.
Mwenendo wa bunge letu na uongozi wa bunge la Tanzania umejianika wazi zaidi katika bunge lililopita juzi tu. Hoja nyingi ambazo ninaona zilikuwa na manufaa kwa watanzania zilizimwa. Lakini hali imekwenda mbali zaidi na hata kuamua kutorusha matangazo ya moja kwa moja ya bunge. Maana yake ni sawa na kusema, tuchagueni tuwatumikie lakini msituangalie. Huu ni upofu ambao ninaamini Mungu anawapiga baadhi ya watala au viongozi wetu ili watanzania mtambue kuwa hali si shwari. Na isiishie kutambua tu ila pia na kuwatambua wale wanaosababisha hali kutokuwa shwari.

Unaweza kumlaumu Spika, Naibu spika au yeyote yule. Lakini tatizo ni zaidi ya mtu au watu japo nao wanaweza kuwa na matatizo yao. Tatizo ni mfumo mzima wa utawala. Uzuri wa mifumo ya namna hii huwa lazima iwe na mwisho. Isingekuwa hivyo akina Adolf Hitler, Adi Amini Dada, Mobutu Seseko na wengine wengi yasingewakuta yaliyowakuta. Kuongezewa ulinzi kwa kiongozi au mtawala, akilindwa dhidi ya anaowatawala au kuwaongoza ni sifa ya udikteta. Madikteta ndiyo ambao hujilinda dhidi ya wananchi. Leo kaongezewa huyo, kesho je? Je kesho kutwa? Ikifikia watawala au viongozi karibu wote kutakiwa kuongezewa ulinzi tafsir yake ni nini? Si rahisi tukafika huko japo hizi si dalili nzuri.
Wapo baadhi wanaoamini kuwa serikali inayoundwa na Chama Cha Mapinduzi inaweza kubadilika na kuwatendea haki watanzania na kujenga mfumo mzuri wa kimaendeleo. Bado wapo baadhi wanaodhani kwamba mtu fulani au kiongozi fulani akiwa rais kupitia CCM hali inaweza kubadilika. Siwapingi ila nina uhakika huo utakuwa muujiza wa ajabu sana. Kwangu mimi hata akishuka malaika leo, akasema anataka kuwa rais kupitia chama cha mapinduzi, itakuwa na kazi nzito sana ya kunishawishi na kunithibitishia kuwa kweli yeye ni Malaika. Maana mtazamo wangu ni kwamba akishuka Malaika leo kitu cha kwanza, atakuwa na orodha ndefu ya mafisadi na kuanza kuwashughulikia mara moja.

Kwa nini nazungumzia kushuka kwa Malaika  kitu ambacho si rahisi kutokea? Ni kwa sababu mfumo wa chukua chako mapema kwa sasa kwa kiasi fulani unatisha. Watu wengi wanaogopa, wengine wameamua kukaa kimya, wengine wameamua kuwaunga mkono hata kama nafsini mwao wanaona hatia.  Wapo wanaoogopa kujikuta au kukutwa msitu wa mabwe pande.
Ikiwa unaogopa kusema au kuzuia hivi kweli hata kwenye kura unashindwa? Hapana unaweza kusema hapana kupitia kura yako. Wengine mtasema “oooh watachakachua”. Hiyo huwa haiwezekani, ila inawezekana tu pale ambapo wewe hupigi kura au ukiuza kadi ya kupigia kura. Watanzania karibu wote tulio wazalendo na wenye nguvu ya Mungu juu yetu tukisema hapana kupitia boksi la kura ninakuhakikishia kuchakachua haiwezekani.

Hata wao wana akili. Hata kama una ujasiri kiasi gani, watu zaidi ya asilimia 80 wasipokuchagua huwezi kujaribu kuchakachua kwa sababu hawa asilimia 80 wana mawazo yanayofanana. Kura zao zikichakachuliwa kila mmoja akianza kuhoji ghafla watajikuta wapo zaidi ya asilimia 80 wanahoji. Sasa unaweza kuelewa nini kinaweza kutokea, kunapokuwa na kundi kubwa linalohoji. Kwani katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki ilikuwaje? Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM hakumpongeza Mh Joshua Nassar? Alimpongeza. Tukiamua kwa nafasi nyingine yoyote hata ya urais, nina kuhakikishia pongezi zitatolewa tu, iwe kwa kupenda au la.
Kanuni hiyo hiyo ndiyo itakayotumika ukiamua kupiga kura ya kuitetea Tanzania. Unadhani kwa nini ratiba za kufungua vyuo nchini zilibadilika kipindi cha uchaguzi uliopita hali ikijulikana kuwa wanavyuo wengi walikuwa wamejiandikishia vyuoni. Muda wa kufungua vyuo ulisogezwa mbele ili tu uchaguzi upite huku wanavyuo wengi wakikosa nafasi ya kupiga kura. Sasa tambua kuwa hata aliyekuwa mwaka wa kwanza wakati huo hatakuwa chuoni mwaka 2015. Kwa hiyo mabadiliko hayakwepeki.

Dk Steven Ulimboka muda mfupi baada ya kuokotwa katika msitu wa mabwepande akiwa hoi. Unadhani ulinzi kwa huyu ndugu ungepaswa kuwaje ukilinganisha na Anne Makinda?
 
Wengine watasema “kwani hata hao wengine si wanadamu tu” Ni kweli ni wanandamu lakini ambao hajawahi kuunda serikali. Wengi wanaosema hayo huwa ama ni walewale wa Chukua Chako Mapema au uelewa mdogo. Hakuna zaidi ya hapo. Wito wangu kwa watanzania wenzangu, hatma ya nchi yetu ipo mikononi mwetu. Hatupaswi kukata tamaa. Ukijua hilo ni lazima pia uelewe kuwa hakuna jambo zuri lisilo na gharama. Ila siku zote haki hushinda uovu. Hata kama tunatekwa, tunateswa na kutupwa katika msitu wa pande bado ninaamini tutashinda.
Inawezekana CCM wamefanya mazuri mengi lakini kwa sasa hatuna budi kubadili mfumo wa utawala. Ili watu kama akina Samweli Sitta, Dk Harison Mwakembe, Dk Steven Ulimboka na wengine wengi wafurahie kuwatumikia watanzania kwenye mfumo mpya ambao ninaamini utawajali. Usipowajali mchezo wetu ni uleule. Tunafanya mabadiliko mengine na kuweka mfumo mwingine mpaka hapo tutakapoupata huo tunaoutaka, kuliko kuendelea kubaki na huu uliopo.

Mungu isaidie Afrika, Mungu iokoe Tanzania
George Adriano

0715 182 106

0 comments:

Post a Comment