Saturday, March 30, 2013

MAAFA HAYA HAYAKUSTAHILI KUTOKEA

Kwanza nimesikitishwa sana na taarifa za kuporomoka kwa jengo la orofa 16 jijini Dar es Salaam. Nimejisikia uchungu kwa watu kupoteza maisha. 

Jambo la kwanza lililokuja akilini mwangu kabla hata ya taarifa zinazoonesha uzembe na ufisadi nilijisikia AIBU. Aibu kwa taswira ya nchi yetu katika jamii ya kimataifa.
Jengo linaporomoka pasipo kuwa na tetemeko, pasipokuwa na kimbunga au upepo na hakuna tsunami. Kama hali ni hii itakuwaje siku likitokea tetemeko au kimbunga/upepo?
Ni wakati wa watanzania kuwa na jicho la tatu la kuingalia nchi yetu, jicho la tatu la kuangalia viongozi wetu na hata wataalamu wetu.

Taarifa zilizopo hadi sasa, inaonekana kuna uzembe au ufisadi wa kiuongozi,kiutaalamu na hata kiteknolojia.

Kwanza inaonekana orofa hiyo ilipaswa kuishia orofa 9 na si 16

Pili, Vifaa vilivyotumika kujengea ikiwemo vyuma/nondo na hata zege haikuwa ya viwango vinavyostahili

Tatu, utawala au uongozi na mamlaka husika haikutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha ubora wa jengo na zaidi sana urefu wa jengo.

Nne, hata baada ya orofa kuporomoka, bado tumekuwa na vifaa duni kupindukia na hata kukosekana kabisa kwa vifaa vya kuokolea.

Hili si suala dogo maana watu wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa. Mali zimeharibika yakiwemo magari n.k Na kibaya zaidi hata baada ya watu waliokuwa wamekwama katika vifusi kupiga simu kuwa wamenasa, hatuna vifaa na watu wasamaria wema wakitumia mikono kuondoa vifusi? Hii ni aibu isiyofikirika

Nilipotazama BBC na vyombo vya kimataifa jinsi vinavyoripoti, niliumia sana wanapotaja kuwa Tanzania hakuna vifaa vya kuokolea waliokwama kwenye vifusi. Hakika! kama watanzania tutaendelea kuwachekea watawala na viongozi wazembe, hali si shwari.

Nimekuwa nikijaribu kufikiri aina ya adhabu ya kuwapatia wale wote watakaothibitika kuwa walifanya uzembe katika suala hili, nimekosa! Sioni adhabu ambay ni size yao. Adhabu zote naziona ndogo...

Nimejaribu sana nisiandike mengine ya kuoanisha na hili tukio... Nitaeleza naendelea kutafakari zaidi...

Dk George Adriano

1 comment:

  1. Inasikitisha, usimamizi uanzie chini raisi hawezi kuwa kila mahali

    ReplyDelete