Ni wiki jana tu tulipata taarifa za Mkoa wa Mbeya kupiga marufuku uuzwaji wa CD na DVD zinazokashifu dini nyingine. Wengi walifurahia hatua hiyo hasa wapenda amani na wenye akili timamu. Wengine walidiriki kusema kuwa Mbeya wameonesha njia kwa mikoa mingine. Kamati hiyo ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa mbeya ilipokea pongezi nyingi tu kutoka kwa watanzania wengi wapenda amani.
Tamko la kamati halikuwa linamuomba mtu eti tafadhali acha kufanya hiki, No. Kamati ilitoa tamko wazi kwa ukali unaostahili wa kupiga marufuku aina mbalimbali za uchochezi wa kidini, ikawaasa wananchi, waandishi wa habari na vyombo vya habari nini wafanye na kipi wajiepushe nacho. Lakini pia ikatoa mwongozo wa nini cha kufanya unapokutana na chochezi hizo. Kwa mfano iliwataka wananchi kupeleka nyaraka, vipeperushi CD au DVD hizo katika mamlaka za serikali kuanzia ngazi ya kijiji na katika vyombo vya dola hasa polisi.
Kwa ufupi kamati imeona tatizo, imetambua wajibu wake, imechukua hatua. Wengine wamesema kuwa hatua hiyo imechelewa, ok, wana haki ya kusema hivyo lakini ni vema kuliangalia kwa upana zaidi. Hii ni kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya lakini tatizo halipo Mbeya peke yake ila lipo Tanzania. Mbeya kama mkoa ina kamati hiyo ya Ulinzi na Usalama, lakini Taifa lina Idara ya Usalama wa Taifa, ambayo Rais wa nchi anahusika moja kwa moja. Kwa mtazamo wa kawaida tu kati ya hawa wawili nani kachelewa?
Binafsi ninaipongeza kamati hiyo kwa hatua walioichukua. Lakini ninajiuliza hivi Taifa lipo salama? Uongozi wa awamu ya tatu, rais mstaafu Mh Benjamin Mkapa alipiga marufuku mihadhara na mahubiri yote yaliyokuwa yanakashifu dini nyingine. Ninakumbuka mihadhara hiyo ilikoma kwa kiasi kikubwa tu. Sasa hii awamu ya nne si tu mihadhara au mahubiri ila mpaka mapigano na mauaji yenye mrengo wa kidini yanatokea binafsi sijasikia tamko lenye mashiko kutoka kwa Mh rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, zaidi ya salamu za rambirambi tena zilizosomwa na msemaji wa Ikulu.
Ninafahamu na wewe inawezekana unafahamu kuwa rais ni kiongozi mkubwa kuliko wote katika nchi hii kimamlaka. Nguvu aliyonayo rais wa Tanzania si ya kuchezea. Ninaamini kabisa rais yupo kwenye nafasi nzuri ya kuepusha balaa hili lisiendelee. Nikifika hapa huwa najisikia kulia hasa mtu anayekuwa na mamlaka halafu hayatumii kuleta amani ipasavyo. Yaani unakuwa mkali kwa wafanyakazi na madaktari lakini sio kwa wahuni wachache wanaochochea vurugu zisizo na nia njema. Vurugu ambazo moto wake ukiwaka kuuzima si rahisi sana.
Kama sikusikia basi naombeni mnijuze hivi lini Mh wetu alitoa tamko la kukemea chokochoko za kidini kwa uzito unaostahili? Hili la kuomba kushirikiana na FBI lengo lake nini au lina maana gani? Msemaji wa jeshi la polisi amesema huu ni ushirikiano wa kawaida. Akaenda mbali zaidi na kutoa mfano wa ushirikiano kama huo baada ya kulipuliwa kwa balozo za Marekani hapa Tanzania mnamo Septemba 11, 1998. Lakini katika lile kuna uhusiano wa karibu sana na kuhusika kwa Marekani? Hivyo si ajabu wao kushiriki maana ulikuwa ubalozi wao. Na hili la sasa ni jambo la ndani yaani Interna affairs sasa wamarekani wanahusika vipi? FBI wanahusika vipi? Au ndio kila kitu kwa msaada wa watu wa........? Ifike mahali tuimarike na vyombo vyetu.
Hivi alipotekwa, kuteswa na hatimaye kutupwa katika msitu wa pande aliyekuwa kiongozi wa jumuiya ya madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka, mbona FBI hawakuitwa licha ya unyama na ukatili mkubwa aliyotendewa Dk Ulimboka? Kamanda wa polisi kanda maalumu ya Dar es Salaaam alitamka wazi kuwa matukio ya utekaji ni jambo jipya hapa kwetu, hayajazoeleka, sasa kama ilikuwa hivyo kwa nini FBI hawakuhusishwa? Mkoani Iringa mauaji ya mwandishi wa habari yalitokea kwa nini FBI hawakuhusishwa? Kwa nini katika hili lenye harufu mbaya ya udini? Mambo kama haya yanazua maswali mengi yasiyo na majibu yenye uzito unaostahili kwa watanzania na kuwa na mashaka na usalama wetu. Mambo kama haya tunapaswa kuyashugulikia kikamilifu na kuyamaliza sisi wenyewe ili heshima yetu iwe bora katika mataifa mengine na sisi tupaki na amani na mshikamano.
Kwa sasa Tanzania ina mfululizo wa sura mbaya katika jamii ya kimataifa. Uvunjaji wa haki za binaadamu, ukandamizaji wa demokrasia nchini, uonevu juu ya badhi ya vyombo vya habari na mengine mengi tu. Nadhani Mh rais ni vema kuiga kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Mbeya, hata kama ni kwa kuchelewa. Wakati mwingine si mbaya baba kuiga mazuri ya mwanaye.
Binafsi nadhani ni vema japo kwa kuchelewa Mh rais kutoa tamko la kukemea, kuonya na kupiga marufuku kwa mtu yeyote wa dini yeyote na wadhifa wowote kutoa maneno ya kukashifu au kudharau dini nyingine mahali popote.
Pili kupiga marufuku uuzwaji na usikilizaji wa CD au DVD zinazokashifu dini nyingine, au zinazochokonoa na kudharau dini nyingine. Kwa maana ya kwamba kila dini izungumzie mambo yake na iwajenge waumini wake na kamwe isitoe maneno yoyote ya chuki au yanayoonesha chuki dhidi ya dini nyingine. Mh mkuu wa nchi anapokaa kimya au asipoonesha uzito suala kama hili watu wanakuwa na mashaka si tu kwa yanayotokea ila pia hata juu ya muheshimiwa mwenyewe.
Tatu, Mh rais uiagize safu yako ya Usalama wa Taifa, Jeshi la polisi na vyombo vingine vya kiusalama kutochekea au kumuonea huruma yeyote anayechochea uhasama wa kidini kwa namna yoyote ile badala yake wachukuliwe hatu za kisheria mara moja.
Haya yafanyike na yaonekane yakifanyika, kila idara itekeleze wajibu wake kwa mujibu wa sheria na si kuwalea watu wanaochochea chuki za kidini. Si watu wanafanya mihadhara ya uchochezi, wanarekodi na kuweka kwenye mitandao kama You Tube halafu serikali inakaa kimya. Hiyo ni hatari sana.
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mbeya wamefanya jambo jema si mbaya rais ukifuata vyayo. Niwapongeze viongozi wa dini hasa wale ambao wamekuwa mstari wa mbele kukemea chokochoko hizi. Pia niwape pole wale wote waliofikwa na machungu ya kuuawa kwa ndugu zao, Mungu awafariji.
Mh rais, chukua hatua.
Dk George
Tanzania
0 comments:
Post a Comment