Monday, February 25, 2013

Uhusiano Wako Hujengwa Na Wewe Mwenyewe-3


Ni vema utambue kuwa katika uhusiano hasa kwa kipindi cha mwanzo hata jambo dogo lina maana kubwa katika uhusiano. Kusita kueleza kitu, labda kwa sababu umeona hakina haja au si muhimu sana inaweza kuwa tatizo, hasa kama mwenzako naye si muelewa sana. Ni vema kutokuwa na tabia ya kusita sita.
·         Usichoshe
Lakini pia kueleza habari ndefu sana kama haivutii, humchosha mwenzako. Anaweza akawa mvumilivu kwa kukusikiliza, lakini huwa si vema kama unaongea wewe peke yako tu. Unakuwa umetawala mazungumzo kana kwamba wewe ndiyo unajua kila kitu. Mpe na mwenzako nafasi ya kuongea.
Zipo namna nyingi za kuwasiliana;
·         Kuwasiliani kwa maneno ana kwa ana au uso kwa uso
Kuna kuzungumza ana kwa ana, yaani mpo pamoja mnazungumza mkitazamana au mkiwa karibu karibu. Ni fursa nzuri ya kuonesha hisia zako, ila zisiwe ashki. Maneno, matendo na uvaaji wako umtukuze Mungu. Si vema kutegana na kuamshana hisia za ngono, kwa kisingizio cha kuonesha hisia. Muda ambao mnakuwa pamoja kuzungumza na mahali mnapokuwa pia ni vizuri kupafikiria. Hii inategemea na miyenendo yenu si vema kukaa katika mazingira ya kujitega na kujitengenezea mazingira ya kufanya ngono.
·         Kuwasiliana kwa vitendo au ishara ana kwa ana
Vitendo ni njia nyingine ya kuwasiliana. Inaweza kutumiwa na mtu yeyote, ila mara nyingi hutumiwa na watu maalum. Watu wasiosikia au wasiosikia vizuri. Ikiwa rafiki yako, hana uwezo wa kusikia na ikiwa anajua kuzungumza kwa ishara, ingekuwa busara sana na wewe kujaribu kujifunza kuwasiliana kwa kutumia ishara. Upendo haushindwi jambo. Ni furaha iliyoje kuwa na rafiki ambaye mnawasiliana kwa namna ya kipekee. Jifunze ili kufurahia maisha na rafiki yako.
·         Simu
Lakini pia mnaweza kuwasiliana kwa kutumia simu. Maweza mkawa mnatazamana, hii inategemeana na aina ya simu unayotumia, lakini mara nyingi njia hii unaweza ukasikia tu sauti ya mwenzako. Ni njia nzuri ya kuwasiliana japo mara nyingi watu huitumia vibaya na Shetani hutumia njia hiyo kuharibu urafiki. Simu huchochea sana uongo, maana ni rahisi kushawishika kudanganya kwa sababu rafikio hakuoni ulipo. Kumbuka Ibilisi ndiyo baba wa uongo. Kwa hiyo ukidanganya, iwe umeonekana au hujaonekana, Shetani hufanyika baba yako.
·         Barua na barua pepe
Barua au barua pepe ni njia nyigine nzuri ya kuwasiliana. Japo kutumiana barua linaonekana kama kitu kilichpitwa na wakati, ila kina ladha yake katika urafiki. Huweza kutumika hasa kama si jambo la haraka ila ni kujaribu kumuonesha mwenzako kuwa una mjali. Maana hatakuwa akitegemea kupata barua kwa njia ya posta. Barua pepe ni njia rahisi, na haichafui mazingira. Hufikisha ujumbe kwa haraka pia.
·         Mtandao
Mtandao wa kikompyuta unaweza pia kutumika kwa kuongea au kutumiana ujumbe (chat). Vijana wengi sana wanatumia njia hii. Tatizo ni matumizi mabaya ya mtandao wa kompyuta. Wengine wamejuana kwenye mtandao, wamekuwa marafiki, wametafutana, wakakutana na kufanya ngono. Si jambo jema sana kutangaza kwenye magazeti au mtandao, eti unatafuta mchumba. Roho Mtakatifu akusaidie.
Kila unapowasiliana na rafiki au mwenzi wako, zungumza yaliyo mema. Zungumza mambo mazuri. Usipende kukiri udhaifu au kushindwa, aidha kushindwa kwako au kwa rafiki yako. Sema kitu kwa mtazamo wa ushindi na kujaribu kuthubutu. Maneno yako yawe ya kutia moyo na kamwe si ya kukatisha tamaa. Unaposema maneno ya kukiri udhaifu au kushindwa kwa hakika hukujenga wewe katika hali ya udhaifu au ya unyonge au ya kushindwa.  Lakini kikubwa zaidi maneno hayo humfanya rafiki au mwenzi wako, kuvunjika moyo au kutojisikia fahari kuwa na wewe. Unapungumza mvuto wako kwa mwenzako, shauku ya kuwa na wewe inapungua au inafifia na inaweza kwisha kabisa. Kumbuka binadamu tunatofautiana mtazamo, uelewa, tafsiri ya mambo, fikira, n.k.
Kuzungumza kwa kutumia miili au viungo vya miili yetu au kwa kutumia ishara. Namna unavyoonekana usoni, namna unavyotembea, unavyotazama, n.k. “Moyo wa furaha huchangamsha uso; bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka” Mithali 15:13 Ishara zote za mwili ni njia muhimu sana ya mawasiliano katika urafiki. Kwa hiyo kila unalofanya linaweza kuashiria furaha, heshima, shauku, upendo, huzuni, msongo wa mawazo, uchovu, uvivu, hasira, dharau, majigambo, ubabe au kiburi. Mawasiliano mabaya mara nyingi husababishwa na kitu kibaya au hasira moyoni na kutokuwa muwazi. Lakini wakati mwingine ni ujinga tu wa kutojua kujali au kumsikiliza mwenzako. Uvivu wa kujua mwenzako ana hali gani ana hisi nini au ana tatizo gani. Hii hupelekea marafiki kuanza kuhisi kuwa upendo umepungua au umeisha, kumbe ni ujinga tu wa kutojua kuwasiliana.
Sijawahi kuona mtu akimwangalia tu mtu, anasema, ‘aisee naona upendo ndani ya moyo wa huyu jamaa umejaa, mpaka unataka kumwagika’ Upendo ulio moyoni haujulikani na mtu kwa kukutazama tu, kama mwili wako hautoi mawasiliano, japo Mungu huweza kuutambua. Hivyo ili rafiki yako aone upendo ulioko moyoni mwako ni lazima maneno, matendo yako na mwili wako ujae upendo. Mtu mwenye upendo na furaha hawezi kukaa kinyonge kama mkiwa. Au kutazama kwa dharau au kwa kutojali.  Wengi hudhani wanaweza kuonesha kuwa wana furaha hata kama ndani ya mioyo yao kuna huzuni. Usijidanganye, si rahisi kuonesha furaha wakati una huzuni. Hata kama ukijichekesha au ukitabasamu, huwa kuna tofauti na tabasamu au kicheko halisi. Ndivyo, kwa asili ndivyo tulivyo! Ndiyo asili ya maumbile au miili yetu, japo wapo baadhi wanaoweza kuigiza furaha au huzuni, na mtu akashindwa kujua kwamba anahuzuni kwa jinsi anavyoonekana. Hata hivyo baada ya mtu kuwa karibu na wewe kwa muda fulani na kukufahamu jinsi ulivyo, si rahisi sana kumdanganya. Lakini hata hivyo hii haikujengi, itakuumiza tu moyoni wewe peke yako. Binafsi sidhani kama ni afya sana kufanya hivyo, isipokuwa tu pale inapobidi hasa. Na si kwamba udanganye, ila ni namna utakavyoonesha hisia zako ambazo hazitaonesha huzuni n.k. Upendo lazima uwe na matendo na kweli, sasa kumdanganya mwenzako kuwa una furaha kumbe una huzuni, haikosi ni dhambi pia.
Mara nyingi mwanzoni mwa urafiki au uhusiano, mawasiliano huwa yamejaa hisia na hufanyika mara kwa mara. Haupiti muda mrefu pasipo kuwasiliana hata kama hakuna kitu chochote cha kusema. Ilimradi tu muongee maana hujisikia raha au furaha fulani moyoni. Na wengine husema, ‘nataka tu nisikie sauti yako’ Safi, hiyo inapendeza. Lakini mawasiliano katika mahusiano, hupungua kadiri siku zinavyokwenda. Wengi hawajui hasara au matokeo ya kufanya hivyo. Hii hujenga hisia kuwa upendo umepungua, na zaidi sana kufanya hivyo hupunguza utamu wa urafiki. 
Pamoja na uaminifu, au kuwa na uwezo kifedha au kielimu, mawasiliano ni jambo la kwanza na muhimu sana. Ni vema utambue kuwa mawasiliano ndio msingi wa kumjua mtu. Lakini pia mawasiliano ni njia nzuri ya kuonesha upendo wako kwa rafiki yako. Huku maneno yako yakisindikizwa na matendo mazuri, kila siku unayomtendea rafiki yako. Huwezi kufanya kitu sahihi kwa rafiki yako ikiwa humjui vizuri kwa uhalisi wake.
Kila kitu unachomfanyia mtu yeyote, unahitaji matokeo au mwitikio mzuri kutoka kwa yule unayemfanyia kitu hicho. Unafanya kitu au jambo hilo ukitarajia ama mwenzako atajisikia vizuri, atafurahi au atalichukulia kwa namna ambayo itajenga uhusiano wenu. Utakachokifanya ni lazima kiendane na uhalisi wa huyo unayemfanyia jinsi alivyo. Vinginevyo atachukulia tofauti na matarajio yako. Na hivyo kusababisha kitu kingine ambacho hukutarajia, ambacho kinaweza kuharibu uhusiano wenu.
Kwa hiyo ni vema kuwa mwangalifu kwa kila kitu ufanyacho, hasa katika mawasiliano. Lugha unayotumia, namna unavyozungumza na unazungumza nini kwa wakati gani. “Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake; na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!” Mithali 15:23 Anaposema ‘mtu hulifurahia jibu la kinywa chake’ maana yake, ni kwamba, jibu utakalotoa wewe, ndiyo litakalokufurahisha. Haitegemei uliulizwa nini au utaambiwa nini baada ya jibu lako. Kwa hiyo unaweza kuamua kufurahi au kuhuzunika kwa kuamua ni majibu ya namna gani utoe. Ukitoa majibu yenye... Itaendelea sehemu ya 4 

Dk George
adrianog03@yahoo.co.uk
Dodoma
Tanzania

0 comments:

Post a Comment