Wednesday, February 19, 2014

Kukata Tamaa Kunaua Taifa




Hii ni sehemu ndogo tu ya kitabu ninachoandika, juu ya watanzania, waafrika na viongozi wetu. Watu wakikata tamaa matdhara yake ni makubwa sana... Mtu aliyekata tamaa hasa katika mtazamo wa kisiasa, anaweza kupatwa na mambo matatu... na hapa naeleza mojawapo:-

Tatu, mtu aliyekata tamaa ni rahisi kuona kila kitu ni sawa maadamu anaona wengine wanafanya hivyo. Ni rahisi kukubali chochote kama umekata tamaa ya kukipata ulichotamani kupata. 

Kwa hiyo kwa kuwa umekosa matumaini ya kupata au kuifikia ndoto yako kwa sasa unakuwa huna kitu ndani yako. Chochote kinachotokea mbele yako waweza kukiona kizuri tu. Linapokuja suala la siasa, hapa ndiyo uhitaji wa vyama vya siasa makini unakuja. Watu wakikata tamaa na chama kimoja bas pawepo kingine kilicho makini. Hiki nacho kikiwachosha waweze kwenda kwenye kingine kilicho makini na kitakachowapa matumaini.

Ni hatari watu wakichoshwa na chama tawala wakakata tamaa halafu kusiwepo na chama makini cha upinzani. Wakati mwingine ni hatari maana watu watakichagua chochote kilichopo hata kama hakina lolote la maana, kwa sababu tu wamechoka na wamekata tamaa. 

Ndiyo maana upo umuhimu wa wanazuoni, wasomi na wote waliobobea katika masuala ya siasa kuhakikisha wanatoa mchango wao wa dhati katika kusaidia vyma vichache, hususani viwili katika Taifa ili chama kimoja kinapokuwapo madarakani, nje kuwepo na kingine kinachoweza kuwasaidia wananchi wakati kilichopo madarakani kinapochoka. 

Mara nyingi mfumo wa namna hii ni mzuri maana hutengeneza uwajibikaji wa chama kinaposhika dola. Maana kinajua kuwa nnje kipo kingine ambacho pia ni makini na kikikosea wananchi wanaweza kukichagua hicho pasi na shaka.

Chama kilichopo madarakani kinapojaribu kukidhoofisha chama cha upinzani hasa kinachoonekana kwa kiasi fulani kuwa makini maana yake ni kutaka kuondoa upinzani wenye maana. Maana yake ni kuwavunja moyo na kuwakatisha wananchi tamaa ili pale kinapokosea wananchi wasipate pa kukimbilia. 

Na hiyo ni hatari kwa Taifa, maana hali ikiwa hivyo wapo watawala watakaoifanya nchi kama mali yao, wakijua wananchi hawana pa kukimbilia. Au wakijua hata wakikichagua kingine wao wanakuwa tayari wamejenga misingi yao ya ubabe, wizi wa kura na uminyaji wa demokrasia na hivyo huendelea kushika dola. 

Sasa hatari yake huwa hivi: Nchi inapokuwa haina chama cha upinzani ambacho ni makini, chenye watu wengi katika Taifa, hata kinaponyanyaswa, kukandamizwa na kuonewa kinaweza kisichukue hatua yoyote, kitakuwa kinaogopa kwa sababu hakiungwi mkono vya kutosha. Na hapo mtaendelea kutawaliwa na msiowataka na mnaweza kuishia msikokujua pia. Hatari ya jambo hili si ndogo hata kidogo.

Uzalendo wa wananchi unaweza kupungua na hata kupotea kabisa. Watu taratibu huanza kuwadharau viongozi wao na wakati mwingine kutoheshimu kanuni zinazowekwa, si kwa sababu kanuni hizo ni mbaya ila wakati mwingine ni kwa sababu tu hawampendi kiongozi au uongozi huo. 

Si rahisi kusonga mbele kiuchumi mkiwa na hali kama hii. Si rahisi kupigana na umasikini kikamilifu unapokuwa na raia wasio na hamasa ya kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya Taifa. Hapa ndiyo utawasikia baadhi ya watu wakisema, “sijui kwa nini nimezaliwa hapa.” Wanalaumu kuzaliwa katika nchi yao. Mkishafika hapo uwe na uhakika mmefika msikokujua.

Hulka ya mtu aliyekata tamaa ya kuweza kuona chochote kama kitu kifaacho, inaweza kuliangamiza Taifa hasa kunapokuwa hakuna chama makini kilicho nje ya dola. Maana siku inaweza kufika wananchi wakaamua kukichagua chama dhaifu na hali inaweza kuwa mbaya zaidi, kiuchumi kisiasa na hata kijamii.

Ni vema uzalendo ujengwe si kwa kukipamba tu chama kilichopo madarakani. Uzalendo ujengwe kwa kutoa mchango unaostahili katika kuimarisha chama kimojawapo kilicho nje ya dola pale inapohitajika. Lakini pia uzalendo ujengwe si tu katika kukishambulia chama tawala ila pia kwa kutoa mchango unaojenga ustawi wa Taifa kwa chama kilichopo madarakani pale inapohitajika. Msomi akiweza kutoa ushauri wa kujenga jambo lenye maslahi kwa Taifa bila kuangalia amelipeleka kwenye chama kilicho madarakani au kilichopo nje ya madaraka ina maana nzuri sana. Na hapo ndiyo tunasema, ‘Taifa kwanza halafu chama baadaye.’

Taifa kwanza na chama baadaye, haina maana ni kutukuza chama tawala na kudharau chama cha upinzani. Taifa kwanza na chama baadaye haina maana ni kutukuza chama cha upinzani na kukidharau chama kilichopo madarakani. Taifa kwanza na chama baadaye maana yake ni kuwa na uwezo wa kusema kweli bila upendeleo, hasa wa kichama. Ni uwezo wa kukishauri chama tawala na vilevile ukaweza kukishauri chama pinzani katika kujijenga, kwa maslahi ya Taifa. Ni hali ya kuweza kukosoa jambo baya linapofanyika bila kujali limefanywa na chama gani. Huo ndiyo uzalendo wa kweli, na si uzalendo wa hisia kama wengi walio nao.

Kwa hiyo tukitaka kuondokana na ugumu wa maisha yako ni lazima ubadili mfumo wako wa maisha kwa mwelekeo chanya. Huwezi kufanya kitu kilekile kwa namna ileile na ukategemea kupata matokeo tofauti.

Nasubiri maoni yako, au ushauri wako
George Adriano

2 comments:

  1. Umezungumzia mambo ya msingi sana kaka. Nadhani ni muhimu sana article kama hizi kuandikwa na kusambazwa kwa namna ambayo inaweza kuwafikia watanzania wengi zaidi, People are looking forward for changes but first they must be liberated in mind.

    ReplyDelete