Udikteta
ni
mfumo wa kiutawala ambao mtu mmoja au kikundi kidogo cha watu huwa na mamlaka
yote katika nchi au Taifa ambayo mara nyingi huyapata, kwa kutumia nguvu. Ikiwa
amepata madaraka kwa njia ya demokrasia ili awe dikteta ni lazima endeshe nchi
kinyume na misingi ya demokrasia. Kwa hiyo dikteta hafuati kanuni za
kidemokrasia na wala si lazima afuate sheria halali za nchi.
Kiongozi dikteta si
lazima apendwe na watu. Si lazima atekeleze sera mlizojiwekea. Dikteta anaweza
kufanya au kuwafanyia lolote ambalo anaona linafaa, kwa manufaa yake au na watu
wake wachache.
Wapo baadhi ya
watanzania wametamka, wengine kwa siri na wengine wametamka wazi kabisa kuwa ni
vema wawe na Rais dikteta. Wanataka Rais dikteta. Haina maana hawapendi amani
na utulivu ila hoja ni kwamba wamechoshwa na mafisadi, na wizi wa mali za umma
na kutokuwajibika. Kwa hiyo wanataka Rais dikteta atakayepambana na mafisadi
katika nchi. Wanahitaji dikteta wa kupambana na rushwa katika Taifa.
Baadhi ya watanzania
wanahitaji dikteta atakayewatia watu adabu ili waondokane na uvivu; ili watu
wawe wawajibikaji na hatimaye kujenga Taifa lao. Hawataki Taifa lenye watu
legelege.
Dhana hii imejitokeza
baada ya kuibuka na kuibuliwa kwa vitendo lukuki vya kifisadi, rushwa na
mikataba mibovu yenye kila harufu na rangi ya rushwa, na haya yakifanywa na
watu waliopewa dhamana ya kuiongoza nchi, yaani viongozi.
Rushwa zimetajwa kwa
baadhi ya mawaziri na wengine kufikia hatua ya kujiuzulu nyadhifa zao. Rushwa
kwa viongozi waandamizi wa serikali katika wizara mbalimbali na hata mashirika
na taasisi za umma. Wapo waliofikishwa mahakamani.Wapo waliokutwa na hatia ya
matumizi mabaya ya madaraka na wakaadhibiwa kwa kifungo na wapo walioonekana
kutokuwa na hatia kisheria na kuachwa huru.
Dhana ya kuhitaji
dikteta ni dhana iliyokuja katika mawazo ya baadhi ya watanzania baada ya kuona
kana kwamba hakuna suluhu juu ya mwelekeo wa nchi. Wananchi wengi wanaona kuwa
wao hawana nguvu wala uwezo wa kuwashughulikia viongozi au watawala wao hasa
wale walio wabovu.
Wasomaji wangu hizi ni sehemu ndogo za ninachokiandika.... nahitaji maoni yenu.
George Adriano
0 comments:
Post a Comment