Wednesday, March 12, 2014

WENGI HAWAJUI MAANA YA SIASA: WEWE JE?

Nitakuwa na mfululizo wa somo la siasa. Fuatilia hapa.

Siasa ni neno pana nitajaribu kulieleza na kufafanua kwa mwelekeo wa nchi au Taifa. Ninajua wapo wanaodhani katika makanisa na misikiti hakuna siasa. Ukweli ni kwamba utakuwa huelewi tu lakini siasa ipo kila mahali isipokuwa mbinguni na jehanamu.

Kila mahali kuna namna fulani ya uongozi. Iwe ni kanisani, msikitini na hata kwenye familia kuna mfumo wa uongozi na usishangae nikikwambia kuwa kuna siasa pia.

Siasa ni njia au mbinu zinazotumika kusimamia, kuongoza au kutawala Taifa au serikali. Hii ni maana ya moja kwa moja inayohusiana na nchi, au Taifa. 




Kwa upana zaidi, siasa ni namna yoyote inayohusiana na kujenga muunganiko wa mamlaka tofauti zilizopo katika jamii zilizo ndani ya dola; daraja hilo hubeba mawazo kutoka katika jamii na kuyapeleka kwenye dola na vilevile huyatoa kutoka kwenye dola na kuyaleta kwa jamii. Ni kila kitu kinachohusu muunganiko wa kimamlaka kati ya dola na jamii—kati ya viongozi na wanaoongozwa.

Daraja hili la mamlaka hubeba mambo kama matumizi ya madaraka, mgawanyo wa madaraka na uhalalishaji wa madaraka husika. Nani awe na mamlaka kiasi gani, na ayatuamiaje.

Mambo yote haya kimsingi yanatengenezwa na wananchi wenyewe. Wananchi ndiyo wanaamua, je, wawe na Rais au Mfalme? Wanaamua tuwe na Malkia pamoja na waziri mkuu au tuwe tu na Rais na Magavana? Na kila cheo wananchi wanaamua awe na mamlaka kiasi gani. Na wao ndiyo wanasema, mamlaka fulani ni sahihi yawepo. Hata wakisha kumchagua, anapokuja na wazo la kubadili kitu kwa niaba yao, linapaswa kukubaliwa na wananchi. Maana wananchi ndiyo chanzo cha mamlaka ya serikali yao. 


Sasa unaweza ukaona mambo kama yapo tofauti kidogo na ninavyoeleza hapa, ila ninaamini utaelewa. Viongozi wanapochaguliwa na wananchi katika nyadhifa au vyeo au nafasi ambazo wananchi wameziridhia kuwepo katika Taifa lao, kimsingi wao ndiyo chanzo cha mamlaka hayo. Sasa kiongozi akishapewa mamlaka anakuwa na wajibu wa kuyatumia. Ifahamike kuwa lengo la kuweka mamlaka hayo ni ili yatumike kwa maslahi ya Taifa na si vinginevyo. Kiongozi kupewa mamlaka ni ili kujenga nidhamu katika utaratibu wa uendeshaji wa mambo katika nchi au Taifa.

Nadhani unafahamu kuwa sisi si malaika, tunaweza kukosea. Pamoja na kuweka sheria, kanuni na taratibu zinazoweza kumbana kiongozi lakini haziwezi kuwa sahihi na sawa kwa asilimia mia moja. Lakini pia hata uwekwaji wa sheria hizo huanza kwa kuwa na watu wachache wanaofanya kazi hiyo, kwa hiyo ni wazi kuwa hawawezi kuweka kila kitu kiwe kikamilifu kwa asilimia mia moja. Na tena upo pia uwezekano wa kujipendelea katika madaraka hayo hasa kama wapo katika nafasi ya kushika madaraka hayo.


Kwa hiyo Taifa lenye watu wa aina tofauti za mtazamo, viwango tofauti vya elimu na hata nia tofauti katika shughuli zao za kila siku hujikuta wapo katika mfumo wa maisha unaoongozwa na ‘mamlaka’ iliyopo. Hivyo maisha huendelea kusonga siku hadi siku, mambo hubadilika, mengine kurekebishwa na mengine mapya huanzishwa na mfumo wa uongozi unaendelea kuwepo.

Kwa wananchi kuendelea kukaa au kuishi na mfumo huo wa uongozi au mamlaka, maana yake wamekubali. Kisiasa wamekubali aina ya mfumo walio nao. Kwa hiyo mfumo huo unakuwa na nguvu ya kutunga na kutekeleza sera, sheria, kanuni na taratibu mbalimbali. Unaweza usizipende zote lakini wanaweza kulazimisha ziwepo kwa sababu ama ya mamlaka au kwa sababu ya wengi wamekubali hivyo.


Dola katika nchi inakuwa na nguvu kuliko wananchi si kwa sababu ni kweli ina nguvu kuliko wananchi ila ni kwa sababu wananchi wamekubali iwe hivyo. Kumbuka chanzo cha mamlaka katika nchi ni wananchi wenyewe. Na hapa ndiyo utawasikia watu wakisema, “Nguvu ya umma.” Kwa sababu mamlaka ya serikali inatoka kwa wananchi wenyewe.

Tayari nchi au Taifa lina pande mbili. Upande wa kwanza ni wa watawala au viongozi waliopewa mamlaka na wananchi na upande wa pili ni wa wananchi walitoa mamlaka yao kwa watawala au viongozi. Japo wote wananonekana kuwa na nia moja na lengo moja la kuwa na Taifa la aina fulani lakini ukweli ni kwamba tayari haya ni makundi mawili yanayoweza kuwa na mtazamo tofauti kabisa.


Wakati wananchi wanaweza kuwa na nia ya kuwa na viongozi imara, bora na wenye nia ya kujenga mazingira mazuri kwao, watawala au viongozi wanaweza kuwa na nia ya kuendelea kutawala. Kwa nini? Kwa sababu wameonja mamlaka na wameona ni mazuri kwa maisha yao na familia zao pia.

Kumbuka watawala au viongozi ni watu tu kama wewe. Mvutano unaweza kutokea hasa pale makundi haya mawili yanapokuwa yametofautiana. Wananchi watataka mazingira mazuri kwa ajili ya maendeleo yao, na watawala wanaweza wakawa wanashughulikia zaidi maendeleo yao binafsi. Wakati wananchi wanataka maji safi ya kunywa, watawala wanataka magari mazuri ya kifahari. Kwa hiyo angalau umeanza kuona picha ya utofauti kati ya watawala na watawaliwa.

Hali hiyo huweza kujenga dhana ya kuwaondoa watawala hao na kuwaweka wengine. Hapo ndiyo watu wengine hujitokeza katika jamii wakitaka kupewa mamlaka.Watawala hutaka waendelee kutawala na wananchi huwataka watawala wengine. 


Utaratibu uliokubalika ukawekwa wa nanma ya kubadili viongozi/watawala na hata kubadili mfumo kabisa. Hii ikiwa ni pamoja na kupokezana madaraka, au kuachia madaraka ili wapewe watu wengine na hata kufikia kupewa si tu mtu mwingine ila chama kingine. Shughuli zote hizi, zinazopelekea kuwapo kwa aina fulani ya watawala au viongozi, utekelezaji wa sera, mipango, sheria, kanuni na taratibu, ndiyo siasa. Kwa mantiki hii sidhani kama kuna mtu anaweza kukwepa siasa.

0 comments:

Post a Comment