Kwa ufupi hakuna
mtu anayeweza kukwepa kuathiriwa au
kuguswa na masuala ya uongozi. Haijalishi unafanya kazi halali au haramu huwezi
kukwepa athari za siasa. Unaipenda nchi yako au huipendi siasa na masuala ya
uongozi wa nchi yako una sehemu kubwa katika kujenga mazingira ya nchi yako.
Tunayo mifano mingi ya
nchi na mataifa mbalimbali yenye vita na machafuko ya kivita. Tunaona matokeo
yake wazi kabisa. Wapo wanawake, watoto, wazee na hata vijana wanaoteseka na
hata kufa au kuuawa. Wengine hupoteza makazi yao na kulazimika kuishi katika
vichaka na mahema huku wakikabiliwa na
ukosefu wa chakula na maji pamoja na huduma nyingine za kijamii.
Wengine hufa kwa
magonjwa kunakosababishwa na mazingira hatarishi na ukosefu wa huduma za afya
na madawa. Swali la kujiuliza ni Je, hao wanaokumbwa na hayo walipenda hivyo?
Fikiri juu mtoto anayekufa
kwa sababu ya njaa nchini Sudani ya kusini eti kwa sababu ya vita.
Haijalishi wewe ni
nani, haijalishi unafanya nini au unamiliki nini, linapokuja suala la siasa
kumbuka una wajibu wa kufanya. Kila mtu katika Taifa lake ana wajibu fulani juu
ya siasa ya Taifa lake. Ni kukosa tu uelewa au ni kukata tamaa ndiko
kunakowafanya watanzania na hata waafrika kwa ujumla kusema, hawajihusishi na
siasa. Haijalishi unajihusisha au la, siasa hugusa maisha yako ya kila siku.
Yaani hapa haina haja ya kujua kama wewe unawajibika katika masuala ya siasa ya
nchi yako au la, siasa itakugusa tu.
Inawezekana nisikueleze
wajibu wako binafsi hasa ila ukweli usiopingika ni kwamba, wewe una wajibu
katika siasa. Kila mtu analo kusudi lililosababisha kuzaliwa au kuishi katika Taifa
ulilozaliwa au unaloishi. Ikiwa unaishi katika Taifa lako, katika Taifa
ulipozaliwa ni vema kuchukua nafasi yako ya kulitumikia Taifa lako pasi na
shaka wala hofu. Tekeleza wajibu wako, fanya likupasalo kufanya kwa maslahi ya
Taifa lako.
Kwa hiyo hakuna mtu
hata mmoja asiyehusika na uongozi au siasa. Wapo baadhi ya watu wanaodhani kuwa
siasa haiwahusu. Uongozi unamhusu kila mtu bila kujali dini, kabila au rangi ya
ngozi yake. Mfumo wa uongozi au utawala kwa sehemu kubwa unachangia kujenga au
kubomoa maisha ya watu wake kwa namna moja au nyingine. Na wakati mwingine
uongozi unaweza kujenga watu wa tabaka fulani na kubomoa au kuathiri vibaya
maisha ya tabaka jingine.
Kwa hiyo usishangae mtu
akisema nafasi iliyopo kati ya tabaka la walionacho na wasionacho inazidi
kuongezeka katika uongozi huu ukilinganisha na uongozi uliopita. Mfumo wa
uongozi au utawala unaweza hujenga misingi ya maisha ya Taifa na unaweza
kuiharibu na kujenga misingi mingine isiyofaa.
Pamoja na uongozi au
utawala kuwa na uwezo mkubwa wa kujenga au kuharibu mifumo fulani ya Taifa
lakini wananchi wake kwa ujumla wao wana nafasi kubwa ya kukubali au kukataa
mfumo wasioutaka. Kwa hiyo binafsi sipendi kulaumu tu uongozi au utawala japo
una sehemu yake ya kuwajibika ila wananchi wenyewe wana nafasi ya kuhakikisha
wanajenga mfumo wananoutaka wao wenyewe.
Na hapa ndipo ile dhana
ya kulaumu huwa inakufa. Maana huna sababu ya kulaumu mtu mwingine wakati wewe
mwenyewe una uwezo na unaweza kusababisha unayoyataka yatokee. Wananchi katika
nchi yoyote duniani siku zote wana uwezo wa kusababisha wanayoyataka yatokee
japo mara zote huwa kuna gharama zake.
Kwa hiyo kukiwa na
mfumo mbaya wa uongozi katika Taifa uwe na uhakika kuwa hali hiyo
hukubaliwa na wananchi wenyewe. Na
ukiona nchi inaendelea na kustawi basi ujue wananchi wake ndiyo sababu wa
kutokea hayo mazuri unayoyaona.
Nimekuwa nikimsikiliza
Rais wa marekani mwenye asili ya Afrika, Barrack Obama. Mara kadhaa amekuwa
akisema, hatua au mafanikio waliyoyapata Wamarekani yameletwa na Wamarekani
wenyewe. Lakini hapa kwetu Tanzania, kwa mfano; unaweza kumsikia kiongozi
akitamka wazi tena hadharani kuwa, maendeleo yameletwa na chama chake.
Kwa mtu mwelewa, tayari
unapata picha ya aina ya viongozi mlio nao. Kwangu mimi kusema, ‘maendeleo ya
watanzania yameletwa na chama fulani’ ni kuwadharau wananchi. Maana nitajiuliza
kama chama hicho ndiyo kimeleta maendeleo, wananchi walikuwa wapi na wanafanya
nini? Siku zote maendeleo ya nchi huletwa na wananchi wenyewe.
0 comments:
Post a Comment