Nitakuwa na mfululizo wa somo la siasa. Fuatilia hapa.
Siasa ni neno pana
nitajaribu kulieleza na kufafanua kwa mwelekeo wa nchi au Taifa. Ninajua wapo
wanaodhani katika makanisa na misikiti hakuna siasa. Ukweli ni kwamba utakuwa
huelewi tu lakini siasa ipo kila mahali isipokuwa mbinguni na jehanamu.
Kila mahali kuna namna
fulani ya uongozi. Iwe ni kanisani, msikitini na hata kwenye familia kuna mfumo
wa uongozi na usishangae nikikwambia kuwa kuna siasa pia.
Siasa
ni njia au mbinu zinazotumika kusimamia, kuongoza au kutawala Taifa au
serikali. Hii ni maana ya moja kwa moja inayohusiana na nchi, au Taifa.
Kwa upana zaidi, siasa
ni namna yoyote inayohusiana na kujenga muunganiko wa mamlaka tofauti zilizopo
katika jamii zilizo ndani ya dola; daraja hilo hubeba mawazo kutoka katika
jamii na kuyapeleka kwenye dola na vilevile huyatoa kutoka kwenye dola na
kuyaleta kwa jamii. Ni kila kitu kinachohusu muunganiko wa kimamlaka kati ya
dola na jamii—kati ya viongozi na wanaoongozwa.
Daraja hili la mamlaka
hubeba mambo kama matumizi ya madaraka, mgawanyo wa madaraka na uhalalishaji wa
madaraka husika. Nani awe na mamlaka kiasi gani, na ayatuamiaje.
Mambo yote haya
kimsingi yanatengenezwa na wananchi wenyewe. Wananchi ndiyo wanaamua, je, wawe
na Rais au Mfalme? Wanaamua tuwe na Malkia pamoja na waziri mkuu au tuwe tu na
Rais na Magavana? Na kila cheo wananchi wanaamua awe na mamlaka kiasi gani. Na
wao ndiyo wanasema, mamlaka fulani ni sahihi yawepo. Hata wakisha kumchagua,
anapokuja na wazo la kubadili kitu kwa niaba yao, linapaswa kukubaliwa na
wananchi. Maana wananchi ndiyo chanzo cha mamlaka ya serikali yao.
Sasa unaweza ukaona
mambo kama yapo tofauti kidogo na ninavyoeleza hapa, ila ninaamini utaelewa.
Viongozi wanapochaguliwa na wananchi katika nyadhifa au vyeo au nafasi ambazo
wananchi wameziridhia kuwepo katika Taifa lao, kimsingi wao ndiyo chanzo cha
mamlaka hayo. Sasa kiongozi akishapewa mamlaka anakuwa na wajibu wa kuyatumia.
Ifahamike kuwa lengo la kuweka mamlaka hayo ni ili yatumike kwa maslahi ya Taifa
na si vinginevyo. Kiongozi kupewa mamlaka ni ili kujenga nidhamu katika
utaratibu wa uendeshaji wa mambo katika nchi au Taifa.
Nadhani unafahamu kuwa
sisi si malaika, tunaweza kukosea. Pamoja na kuweka sheria, kanuni na taratibu
zinazoweza kumbana kiongozi lakini haziwezi kuwa sahihi na sawa kwa asilimia
mia moja. Lakini pia hata uwekwaji wa sheria hizo huanza kwa kuwa na watu
wachache wanaofanya kazi hiyo, kwa hiyo ni wazi kuwa hawawezi kuweka kila kitu
kiwe kikamilifu kwa asilimia mia moja. Na tena upo pia uwezekano wa
kujipendelea katika madaraka hayo hasa kama wapo katika nafasi ya kushika
madaraka hayo.
Kwa hiyo Taifa lenye
watu wa aina tofauti za mtazamo, viwango tofauti vya elimu na hata nia tofauti
katika shughuli zao za kila siku hujikuta wapo katika mfumo wa maisha
unaoongozwa na ‘mamlaka’ iliyopo. Hivyo maisha huendelea kusonga siku hadi
siku, mambo hubadilika, mengine kurekebishwa na mengine mapya huanzishwa na
mfumo wa uongozi unaendelea kuwepo.
Kwa wananchi kuendelea
kukaa au kuishi na mfumo huo wa uongozi au mamlaka, maana yake wamekubali.
Kisiasa wamekubali aina ya mfumo walio nao. Kwa hiyo mfumo huo unakuwa na nguvu
ya kutunga na kutekeleza sera, sheria, kanuni na taratibu mbalimbali. Unaweza
usizipende zote lakini wanaweza kulazimisha ziwepo kwa sababu ama ya mamlaka au
kwa sababu ya wengi wamekubali hivyo.
Dola katika nchi
inakuwa na nguvu kuliko wananchi si kwa sababu ni kweli ina nguvu kuliko
wananchi ila ni kwa sababu wananchi wamekubali iwe hivyo. Kumbuka chanzo cha
mamlaka katika nchi ni wananchi wenyewe. Na hapa ndiyo utawasikia watu
wakisema, “Nguvu ya umma.” Kwa sababu mamlaka ya serikali inatoka kwa wananchi
wenyewe.
Tayari nchi au Taifa
lina pande mbili. Upande wa kwanza ni wa watawala au viongozi waliopewa mamlaka
na wananchi na upande wa pili ni wa wananchi walitoa mamlaka yao kwa watawala
au viongozi. Japo wote wananonekana kuwa na nia moja na lengo moja la kuwa na
Taifa la aina fulani lakini ukweli ni kwamba tayari haya ni makundi mawili
yanayoweza kuwa na mtazamo tofauti kabisa.
Wakati wananchi
wanaweza kuwa na nia ya kuwa na viongozi imara, bora na wenye nia ya kujenga
mazingira mazuri kwao, watawala au viongozi wanaweza kuwa na nia ya kuendelea
kutawala. Kwa nini? Kwa sababu wameonja mamlaka na wameona ni mazuri kwa maisha
yao na familia zao pia.
Kumbuka watawala au
viongozi ni watu tu kama wewe. Mvutano unaweza kutokea hasa pale makundi haya
mawili yanapokuwa yametofautiana. Wananchi watataka mazingira mazuri kwa ajili
ya maendeleo yao, na watawala wanaweza wakawa wanashughulikia zaidi maendeleo
yao binafsi. Wakati wananchi wanataka maji safi ya kunywa, watawala wanataka
magari mazuri ya kifahari. Kwa hiyo angalau umeanza kuona picha ya utofauti
kati ya watawala na watawaliwa.
Hali hiyo huweza
kujenga dhana ya kuwaondoa watawala hao na kuwaweka wengine. Hapo ndiyo watu
wengine hujitokeza katika jamii wakitaka kupewa mamlaka.Watawala hutaka
waendelee kutawala na wananchi huwataka watawala wengine.
Utaratibu uliokubalika
ukawekwa wa nanma ya kubadili viongozi/watawala na hata kubadili mfumo kabisa.
Hii ikiwa ni pamoja na kupokezana madaraka, au kuachia madaraka ili wapewe watu
wengine na hata kufikia kupewa si tu mtu mwingine ila chama kingine. Shughuli
zote hizi, zinazopelekea kuwapo kwa aina fulani ya watawala au viongozi,
utekelezaji wa sera, mipango, sheria, kanuni na taratibu, ndiyo siasa. Kwa
mantiki hii sidhani kama kuna mtu anaweza kukwepa siasa.